Kitengo cha Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwa kushirikiana na Taasisi ya CHaRA imefanikiwa kutoa elimu ya afya kwa wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Dongobesh, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ustawi, ulinzi na maendeleo ya mtoto wa kike katika jamii.
Elimu iliyotolewa ilijikita katika masuala ya afya ya uzazi na hedhi salama, madhara ya ukatili wa kijinsia pamoja na namna ya kujilinda na kutoa taarifa pindi vitendo vya ukatili vinapotokea. Kupitia mafunzo hayo, wanafunzi walipata fursa ya kuuliza maswali, kushirikishwa uzoefu na kupewa maarifa yatakayowawezesha kufanya maamuzi sahihi yanayohusu afya na maisha yao kwa ujumla.
Aidha, katika tukio hilo wanafunzi wa kike waligawiwa taulo za kike kama sehemu ya kusaidia wasichana kuhudhuria masomo yao kwa uhakika, kuongeza kujiamini na kupunguza changamoto zinazotokana na ukosefu wa vifaa vya kujisitiri wakati wa hedhi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Ndugu Ezekiel Assecheck ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii amesisitiza umuhimu wa jamii na wadau kuendelea kushirikiana katika kulinda haki za mtoto wa kike, akibainisha kuwa uwekezaji katika elimu ya afya ni msingi muhimu wa kumjengea msichana maisha salama na yenye tija.
Kwa upande wake, Carol McDonald kutoka taasisi ya CHaRA ameeleza kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Mbulu katika utekelezaji wa programu zinazolenga kuzuia ukatili wa kijinsia na kuboresha afya na ustawi wa watoto na vijana, hususan wasichana.
Halmashauri inaendelea kupongeza mchango wa wadau wote wanaoshirikiana katika juhudi za kuinua elimu, afya na ustawi wa jamii, na inaahidi kuendeleza ushirikiano huo ili kuhakikisha mazingira salama na rafiki kwa watoto, hasa mtoto wa kike.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.