Na Ruth Kyelula- Afisa Habari
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Kheri James, amewataka Watendaji wa Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu waratibu maonesho ya mara kwa mara yanayohusu mambo ya Lishe kwenye kata zao.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Kheri James, wakati akifungua kikao cha Lishe kwa Watendaji wa Kata, kilichofanyika November 23,2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, kikihudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi, Maafisa Lishe, Kaimu Mganga Mkuu, Watendaji wa Kata pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
"Wilaya nyingine wanafanya ninyi mnashindwa nini?wekeni hapo siku hiyo ni mambo ya kuonesha mambo ya Lishe, aina za vyakula vya vitamini A, mafuta yanayotakiwa, lakini nataka niwaambieni mkitengeneza huo utaratibu wa mara kwa mara na ninyi maafisa Lishe mkishuka kule chini kwenye vijiji, watu wataelewa kwa sababu chakula sisi tunacho kinachotushinda ni nini tule ili tuweze kuimarisha Lishe, kwa hiyo hakikisheni Kila siku ujumbe wa Lishe unawafikia wananchi."
Naye Afisa Lishe wa Wilaya Lutengano Emmanuel, alisema kuwa wadau wa Lishe wanataka kubuni Mbinu ambayo itawafanya wanaume waweze kushiriki na kujifunza ili kupata elimu ya mambo ya Lishe, kuhakikisha kwamba hawakosi kwenye malezi ya watoto lakini kushiriki kwa ujumla katika kupambana na Lishe duni kwa jamii inayowazunguka.
Aidha Afisa Lishe alisema kuwa yapo baadhi ya makundi ya vyakula yakiwemo nafaka,mizizi, vyakula vya asili ya wanyama na jamii ya mikunde, ndizi mbichi, mboga mboga za aina zote,matunda ya aina zote na vyakula vyenye asili ya mafuta, sukari na asali. Alisema maji ni muhimu sana lakini hayapo kwenye makundi ya vyakula ila ni muhimu kuyatumia na wanashauri kitaalamu mtu anywe angalau glasi nane za maji kwa siku kwa mtu mzima ama lita mbili.
Kwa upande wa Afisa Mtendaji Kata ya Maretadu, Saluthary Kossy alisema kuwa amejipanga kwenda kutekeleza maagizo ya Mkuu wa Wilaya na Afisa Lishe kwa kufanya vikao vya ndani,kutembelea vituo vya afya, zahanati kwa ajili ya kukumbusha wakuu wa zahanati na kutoa elimu kabla hawajaanza kutoa huduma kwa wamama wajawazito pamoja na wale wamama wenye watoto chini ya miaka mitano. Na tutatumia elimu kwa vitendo ya kuwaonesha picha na mabango kuhusu Lishe.
Afisa Mtendaji Kata ametoa wito kwa jamii kuzingatia elimu zinazotolewa na wataalamu, zinazotolewa kwa ngazi ya Halmashauri kwa maana watu wa Afya na watumishi wote wa serikali kwa ngazi za kata na vijiji . Na kufuata zile kanuni za masuala ya Lishe kwa ajili ya kujenga Taifa lao la kesho.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.