NA, Ruth Kyelula, Mbulu DC.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Veronica Kessy amewataka maafisa usafirishaji (boda boda), wazingatie sheria na kanuni za barabarani ili kujiepusha na ajali mbalimbali zinazotokana na kutozingatia sharia za barabarani.
Hayo yalisemwa jana October 18, 2024, na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Veronica Kessy, wakati akisikiliza kero za maafisa usafirishaji maarufu kama boda boda katika viwanja vya Dongobesh.
Mkuu wa Wilaya akizungumza na waendesha boda boda wa Dongobesh .
“Mimi leo mama yenu nimekuja kuwasikiliza, na katika kuwasikiliza huko kuna vilio nimevisikia, malalamiko hasa upande wa mafuta. Kwahiyo nimeona nije mimi na kamati yangu ya usalama ili tuwasikie changamoto ni nini,’’.
Mbali na hilo DC aliwashauri waendesha boda boda waanzishe SACOS yao itakayowasaidia kwa maisha ya baadae ili waweze kukuza mitaji yao na kukopeshana fedha kupitia akiba ambayo walikuwa wanawekeza.
Waendesha boda boda wa Dongobesh wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya.
Nao maafisa usafirishaji wa Dongobesh, walisema kuwa changamoto kubwa ni sheli kuwa moja ambapo inapelekea mafuta yakifika yanakaa siku chache na kuisha huku wachuuzi wa reja reja kupigwa marufuku na EWURA kuuza mafuta kwenye vidumu na kusababisha kukosekana mafuta zaidi ya wiki moja.
Mkuu wa Wilaya, Veronica Kessy (wa pili kushoto) akiwa na timu yake.
Baada ya hapo DC alikutana na wananchi wa Dongobesh na kuwaomba wakajiandikishe kwenye daftari la mkazi katika kitongoji chao, ili waweze kupiga kura tarehe 27 novemba, 2024, ili waweze kumchagua Mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa kitongoji na wajumbe wa halmashauri ya kijiji, ambapo zoezi la kujiandikisha linaisha kesho Octoba 20, 2024.
Wananchi wa Dongobesh wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Mbulu.
“Najua mabango mengi yamebandikwa, PA zimepita kutoa elimu, lakini bado na mimi kama Mkuu wa Wilaya nimekuja kutoa elimu kuwasisitiza na kuwaomba twende tukajiandikishe, ili uweze kuitumia haki yako ya kikatiba,haki yako ya kidemokrasia ya kwenda kuchagua kiongozi ambae wewe unamwamini, atasimama kwa ajili ya kitongoji chako ili kusimamia masuala mazima ya maendeleo,kwa ambae bado hujajiandikisha,nenda kajiandikishe ”.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.