Na, Ruth Kyelula – Afisa Habari Mbulu DC.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakar Kuuli, amewaasa wamama wajawazito kuzingatia lishe bora ili kumjenga mtoto aliyeko tumboni aje kuwa bora kwa taifa la kesho.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi, wakati akifungua kikao cha kamati ya lishe cha robo ya pili kuanzia Oktoba hadi desemba 2023. Kikao hicho kilifanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri Januari 29, 2024.
“Kwahiyo suala la lishe tunavyokaa hapa sisi, tunajadiliana mustakabali wa maendeleo ya Halmashauri yetu. Watoto wetu wa baadae waje kuwa na akili, wafanye mambo makubwa kwa ajili ya Nchi yetu.” Alisema Mkurugenzi wa Halmashauri.
Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Jackline David amesema kuwa kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2023, walipata jumla ya watoto wenye utapiamlo mkali saba (7) ambao walilazwa katika kituo cha Afya Dongobesh kwa ajili ya matibabu Zaidi.
Baadhi ya wajumbe wakiwa kwenye kikao cha Lishe .
Aidha bi. Jackline alisema kwa kipindi cha robo ya pili (Oktoba hadi Desemba 2023) waliweza kusambaza matone ya vitamini A, dawa za kutibu minyoo ya tumbo katika vituo vyote 35 vya kutolea huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, waliweza pia kufanya uchunguzi wa hali ya lishe, ambapo jumla ya watoto 27456 walifanyiwa uchunguzi wa hali ya lishe, kati yao 7 walikuwa na utapiamlo mkali na 10 walikuwa na utapiamlo wa kadri.
Aliendelea kusema kuwa kwa kipindi hicho hicho cha robo ya pili waliweza kutoa madini chuma kwa akina mama wajawazito ambapo jumla ya akina mama wajawazito 13104 kati ya 13513 walihudhuria kliniki sawa na asilimia 96.97% walipata vidonge vya madini chuma (FEFO).
Naye Afisa Lishe wa Wilaya, Lutengano Emmanuel, alisema zipo changamoto mbalimbali wanazozipitia ikiwemo muitikio mdogo kwa Watendaji juu ya kuadhimisha siku ya afya na lishe katika vijiji vyao, ushiriki mdogo wa wanaume katika malezi ya watoto, kutokana na kujikita katika ulevi uliokithiri pamoja na baadhi ya wazazi kutozingatia matibabu na kuwa na imani potofu kuwa wamelogwa na hivyo kufanya watoto wenye utapiamlo mkali kutopona kwa wakati na wengine kurudia katika hali ya utapiamlo mkali.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.