Mji mdogo wa Haydom wa Wilayani Mbulu Mkoani Manyara na viunga vyake kwa muda wa wiki hii nzima utakumbwa na burudani kubwa kupitia tamasha la ujasiriamali na michuano ya Kurugenzi Cup ’18 iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Hudson Kamoga.
Pamoja na mada za ujasiriamali kutolewa pia michuano ya soka itakayoshirikisha timu 10 itatimua vumbi kwenye viwanja vya Haydom na kufikia tamati jumapili ya Mei 20.
Kamoga akizungumza wakati wa ufunguzi wa tamasha na michuano hiyo alisema lengo la kuandaa ni kusisitiza uzalendo wa vijana na jamii kwa ujumla kuipenda nchi yao.
Kamoga alisema anatarajia vijana watajinyanyua kiuchumi kwa kufanya kazi kupitia kauli mbiu ya tamasha hilo isemayo wakati wa kuwa mzalendo na kujenga nchi yetu, uvivu ni sumu ya maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga akikagua timu ya Kidarafa FC kwenye ufunguzi wa michuano ya Kurugenzi CUP ’18 inayoshirikisha timu 10 na kufanyika kwenye viwanja vya Haydom ambapo pia kutakuwa na matamasha mbalimbali ikiwemo semina ya ujasiriamali.
Alisema kwa muda wa wiki moja itakayofanyika tamasha hilo kutakuwa na mada mbalimbali za ujasiriamali zitakazotolewa na magwiji mbalimbali waliobobea kwenye uchumi.
“Wilaya ya Mbulu ina fursa nyingi na vichocheo vya kiuchumi hivyo tutawatumia watu maarufu akiwemo mchambuzi wa soka Shafi Dauda ambaye atakuja hapa Haydom,” alisema Kamoga.
Alisema wanatarajia kuibua vipaji vipya tofauti kwenye soka na riadha ili vijana wafuate nyayo za mwanariadha maarufu wa zamani John Stephen aliyeacha historia kwenye michuano ya dunia.
“Kwa muda wa wiki hii nzima kutakuwa na shamrashamra kwenye mji mdogo wa Haydom na wilaya ya Mbulu kwa ujumla ambapo wageni mbalimbali watakuja kwenye tamasha na mashindano haya yatakayohitimishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo siku ya jumapili ijayo,” alisema Kamoga.
Hudson Kamoga akitakiana kheri na mwamuzi kwenye michuano ya Kurugenzi CUP ’18 itakayoshirikisha timu 10 na kufanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Haydom.
Baadhi ya timu shiriki toka dongonesh na kidarafa zikiwa zimebeba ujumbe wa maadhimisho ya wiki ya ujasiliamali wakati wa uzinduzi wa michuano ya Kurugenzi CUP ’18 kwa kufunga bao,michuano hiyo itashirikisha timu 10 na kufanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Haydom ambapo pia kutakuwa na matamasha mbalimbali ikiwemo semina ya ujasiriamali.
Aidha Katibu wa chama cha soka cha wilaya ya Mbulu (MDFA) Joseph Nicodemus alitaja timu zitakazoshiriki michuano hiyo ni Dongobesh FC, Young Boys, Airport SC, Qadesh SC, Mlimani City Lambo FC, Stand United, Makurusa SC, Rema 1,000 na Kidarafa FC ya wilaya jirani ya Mkalama Mkoani Singida.
Nicodemus alisema michuano hiyo itakayofanyika kwa muda wa wiki moja itatumia mtindo wa mtoano na siyo ligi, hivyo timu ikifungwa inatolewa mashindanoni.
Kwenye ufunguzi wa michuano hiyo, timu ya Dongobesh FC iliifunga timu ya Kidarafa FC ya wilayani Mkalama mkoani Singida mabao 2-1 na mchezo mwingine uliofanyika siku iliyofuata timu ya Stend United (Chama la wana) ya Mji mdogo wa Haydom iliifunga Mlimani City ya Ng’wandakw bao 1-0 na mchezo wa kesho jumatano utazikutanisha timu ya Young Boys na Airport SC.
Mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mbulu ndugu Hudson Kamoga akiwa picha ya pamoja na viongozi wa michezo Wilaya, Viongozi wa timu shiriki na wadau wa michezo Wilayani.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.