Na, Ruth Kyelula, Mbulu - DC.
Mkurugenzi wa Uchaguzi ndugu Ramadhani Kailima amewataka Maafisa Habari wa Serikali kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza Julai 1, 2024.
Kauli hiyo aliitoa Juni 15, 2024 wakati akifungua mkutano wa Tume na Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ndugu Ramadhani Kailima, akifungua kikao kazi cha Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri.
“Ndugu Maafisa Habari, uboreshaji huu unahusu kila mwananchi mwenye sifa, Tumieni njia mbalimbali kuelimisha jamii umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza”. Alisema Kailima.
Awali akiwasilisha mada kuhusu uboreshwaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya mpiga kura, Bi. Giveness Aswile amesema zoezi hilo linatarajia kuanza Julai 01, 2024 na baada ya uboreshaji inatarajiwa kuwa daftari litakuwa na jumla ya wapiga kura 34,746,638.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya mpiga kura, Bi. Giveness Aswile akizungumza na Maafisa Habari jijini Dar es Salaam.
“Katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuzingatia matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, daftari linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638 kutoka 29,754,699 ya mwaka 2020 hii ni ongezeko la wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7,” alisema Bi. Givennes.
Bi. Giveness aliyataja mambo yatakayohusika kwenye uboreshaji wa daftari kuwa ni pamoja na kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu 2025 na kutoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo waliloandikishwa awali.
Baadhi ya Maafisa Habari wa Mkoa na Halmashauri walioshiriki kikao kazi cha Tume ya Uchaguzi.
Pia alisisitiza kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao zikiwemo majina na taarifa nyingine, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo na kuukana uraia wa Tanzania au kifo.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.