Na, Ruth Kyelula – Afisa Habari Mbulu DC.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Kheri James ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwa kuwa kinara wa ukusanyaji wa mapato katika mkoa wa Manyara.
Hayo aliyasema wakati akitoa hotuba yake katika kikao cha robo ya pili 2023/24 cha baraza la Madiwani, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri na kuhudhuriwa na Madiwani, timu ya wataalam pamoja na kamati ya usalama, Januari 30,2024.
“Niwapongezeni sana Halmashauri kwa kazi kubwa na nzuri ambayo mnaifanya, ninafurahishwa sana na zoezi la mapato, kwenye mapato kwa kweli hakuna wakufanana nae, hakuna mfano kabisaa hapa ndani ya Wilaya wala Mkoa mzima. Sisi bado tumeshikilia kinara cha mkoa wa Manyara kwenye ukusanyaji wa mapato. Na mimi nataka niwaambieni kwa spidi hii mnanisababisha nitembee kifua mbele kwamba mwaka huu pia Halmashauri ya Wilaya hii itaongoza katika kukusanya mapato katika mkoa wa Manyara.” Alisema Mkuu wa Wilaya Kheri James.
Kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili 2023/24
DC Kheri, ameendelea kushauri kutokana na mvua zinazoendelea wananchi kuweka akiba ya chakula ili hata endapo hawatavuna wawe na akiba ya chakula mvua zikiondoka.Lakini pia amewaasa wananchi kuepuka safari zisizo na ulazima na ikiwezekana kuziepuka kabisa.
Kwa upande mwingine Mbunge wa Mbulu vijijini, Flatei Massay amesema kuwa kutokana na changamoto ya mvua barabara nyingi kuharibika na mawasiliano mengi kukatika,pamoja na madaraja kuchukuliwa,ameiagiza TARURA kufanya utafiti wa haraka ili aombe fedha kutoka serikali kuu kwa sababu katika kata zote kumi na nane hakuna iliyo na unafuu.
Mbunge wa Mbulu vijijini Mhe.Flatei Massay akitoa hotuba yake katika Baraza la Madiwani Januari 30,2024.
“Niwapeni pole sana wananchi ambao wamepoteza ndugu zao kutokana na mafuriko yaliyotokea na maeneo mengi,poleni sana kwa kupoteza familia mana najua kata nyingi watu wengi wamechukuliwa na maji, Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema peponi.” Alisema Mhe. Flatei.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, Mheshimiwa Joseph Mandoo, alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, pamoja na timu ya Wataalamu kwa jinsi ambavyo wameendelea kukusanya mapato ya ndani, ambayo kwayo Halmashauri yetu imeendelea kushika nafasi katika mkoa wa Manyara.
Baadhi ya Madiwani wakifatilia ajenda mbalimbali za kikao.
“Hadi Desemba Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu tumekusanya mapato kwa asilimia 83%, ni jambo la kujivunia. Lakini bado hatutabweteka kwa sababu tunatakiwa tuone fursa mbalimbali zinazowezesha Halmashauri kuongeza mapato ya ndani, lakini kuwezesha kuona fursa fichwa ambazo sisi kama wajumbe wa baraza na wataalamu wetu hatukuweza kuona katika mapato yetu ya ndani.” Alisema Mhe. Mandoo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakar Kuuli alisema kuwa kwa upande wa Halmashauri tunaendelea salama na tunaendelea na makusanyo pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Ijapokuwa hali ya hewa ya mvua si rafiki katika shughuli zetu tunazoendelea nazo za miradi.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.