Na Ruth Kyelula, Mbulu DC.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, imekabidhi jumla ya pikipiki 16 za mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vitatu vya vijana, zenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 45,935,000/= ili kuwawezesha vijana hao kujikwamua kiuchumi.
Akikabidhi pikipiki hizo February 13,2025, katika jengo la Halmashauri, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu, amewataka vijana wanufaika wa mikopo hiyo waweze kurejesha kwa wakati ili vijana wengine waweze kunufaika na mikopo hiyo ya asilimia kumi ya Halmashauri.
Kwa upande wa Mbunge wa Mbulu vijijini, Mhe. Flatei Massay, ametoa msisitizo kwa vijana na wanawake kujitokeza katika fursa mbalimbali zinazojitokeza ili waweze kunufaika na kujikwamua kiuchumi na kuleta maendeleo katika jamii zao.
Baadhi ya Wajasiriamali wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, wakiwa na vitambulisho vyao walivyopewa na Halmashauri.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Joseph Mandoo amesema kuwa vijana waliopata mkopo wakumbuke kurudisha mikopo yao kwa wakati ili wengine waweze kupata mikopo hiyo.
“Sisi Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu tunaendelea kushirikiana na wataalamu pamoja na Madiwani kuendelea kutimiza wajibu wetu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma mbalimbali, Halmashauri yetu iliendelea kushika nafasi ya kwanza kwa miaka mitatu mfululizo kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani, na matokeo haya ndio yaliyotuleta hapa leo, ambapo imetuwezesha kutoa mikopo zaidi ya milioni 594, ambapo kwa sasa tumetoa mikopo ya milioni 204 ikiwemo hizi pikipiki,mikopo ya kinamama na vijana pamoja na watu wenye ulemavu.” Alisema Mhe. Mandoo.
Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakar Kuuli amesema mikopo hiyo ya asilimia 10 itaendelea kutolewa kwa makundi hayo ya vijana pamoja na wanawake, hivyo ni vema ikarudishwa kwa wakati.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakar Kuuli, akizungumza na waliopata fursa ya mkopo wakati wa ugawaji wa pikipiki 16.
Baadhi ya vijana walionufaika na mkopo huo ambao ni kati ya shilingi 204,635,000 zilizokopeshwa na Halmashauri, wameishukuru serikali kwa fursa ya mikopo isiyo na riba, ambayo itawakomboa kiuchumi.
Katika hatua nyingine Halmashauri imekabidhi jumla ya vitambulisho vya utambuzi kwa wajasiriamali 52, kwa awamu ya kwanza.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.