Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Marium Muhaji ametoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kukamilisha kwanza miradi kiporo iliyoanzishwa kwa nguvu ya wananchi kabla ya kuanzisha miradi mipya katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Mariam ametoa maelekezo hayo katika kikao Maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu cha kupitia taarifa ya Ukaguzi wa hesabu za Serikali iliyofanywa na mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo miradi kiporo 11 ni miongoni mwa hoja 13 za CAG katika taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Halmashauri hiyo licha ya halmashauri hiyo kuwa na hati safi kwa miaka mitatu mfululizo.
Amesema kuchewa kukamilisha miradi iliyoanzishwa na wananchi ni kukatisha tamaa jitihada zao za kuanzisha miradi hiyo na pia kuchewesha wananchi kuanza kunufaika na miradi hiyo katika maeneo husika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ukaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu haijakamilisha miradi 11 inayohitaji shilingi milioni 145.723 kati jumla ya shilingi Milioni 293.96 zilzokuwa zimetengwa kwa ajili ya miradi hiyo.
Miradi iliyohojiwa katika ripoti hiyo ya CAG ni pamoja na ukarabati wa Machinjio ya Dongobesh, ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari Bishop Hhando, madarasa mawili katika shule ya sekondari Dkt Olsen, Ujenzi wa maabara na matundu 12 ya vyoo katika shule ya sekondari Kari pamoja na ujenzi wa matundu 12 ya vyoo katika shule ya sekondari Masieda.
Miradi mingine ni ujenzi wa choo katika kituo cha Mabasi Haydom, Ujenzinwa maabara katika shule ya sekondari Bashay, ukamilishaji wa jengo la wagonjwa wa nje katika zahanati ya Endagichan na Ujenzi wa nyumba za watumishi katika zahanati ya Mongo wa mono
Katibu Tawala Mariam Muhaji amesisitiza Halmashauri hiyo kutumia mapato yake ya ndani kukamilisha Miradi hiyo kwakuwa itakapokamilika itasaidia kupunguza lawama kutoka kwa wananchi kwamba Serikali inatelekeza miradi yao na kuanza kunufaisha wananchi.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.