Na, Ruth Kyelula, Mbulu DC
Mganga Mkuu wa Wilaya, Dr. Shadrack Makonda, ameitaka jamii iweze kuwaibua watoto wenye changamoto ya utapiamlo na udumavu kwa kutumia vifaa vya kupima mzingo wa mkono ili kujua mtoto amekonda ama la, kifaa cha kupima udumavu kama ameongezeka urefu ama la na mzani wa kujua uzito wa mtoto.
Mganga mkuu Wilaya,, Dr. Shadrack Makonda, akifungua mafunzo ya Tathimini ya hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano.
Hayo yalisemwa na Mganga mkuu wa Wilaya Dr. Shadrack Makonda wakati akifungua mafunzo ya tathimini ya hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano, kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii, yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri September 24,2024.
Mganga Mkuu,Maafisa Lishe na Wahudumu wa afya ngazi ya jamii wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya mafunzo.
“Lengo ni moja, tuwabaini, tuwagundue watoto wenye changamoto ya lishe ili tuweze kuwasaidia. Kwenye jamii zetu wapo watoto wenye changamoto za lishe, wapo wenye utapiamlo, wapo wenye udumavu, na unakuta mtoto akiwa na changamoto hiyo zipo familia zina mficha. Kwahiyo ninyi ndio wa kuwaibua watoto hao kwa sababu ninyi ndio mnaishi kwenye jamii, mnazijua familia na mnawaona watoto wenye changamoto”. Alisema Dr. Shadrack.
Kwa upande wa Afisa Lishe Wilaya ya Mbulu, Jackline David, amesema kuwa Wahudumu wa afya ngazi ya jamii wamekuwa msaada mkubwa sana kwa kuibua matatizo mbali mbali yanayojitokeza katika jamii ikiwa na pamoja kuwaibua watoto wenye utapiamlo mkali, matukio ya ukatili wa kijinsia yanayoenedelea na shughuli zingine jumuishi.
Aidha Afisa lishe amesema kuwa, elimu wanazozitoa katika jamii zizingatiwe, mfano wanapotoa elimu ya ulaji sahihi wa makundi sita ya chakula lakini pia ameomba washirikiane katika matukio ya kikatili ya kijinsia yanayotokea yasibaki kwenye jamii ili waweze kusaidiana, lakini pia wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapewe ushirikiano.
Afisa Lishe wa Wilaya, Jackline David akitoa mafunzo kwa Wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Naye Afisa Lishe, Lutengano Emmanuel amesema kuwa mafunzo hayo yamefanyika kwa awamu ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2024/2025, na kuhudhuriwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii ishirini na tatu (23).
Lutengano aliendelea kusema kuwa, wahudumu wa afya ngazi ya jamii waendelee kufanya kazi kwa weledi ili waweze kuibua watoto wengi na kuweza kujua tathimini ya hali ya lishe imefikia katika kiwango gani lakini pia anatoa wito kwa watendaji wa vijiji na kata kushirikiana nao ili tathimini ifanyike kwa ukubwa na uzuri.
Afisa Lishe, Lutengano Emmanuel akitoa mafunzo kwa Wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.