Mkuu wa Mkoa wa Manyara,Bi. Queen Sendiga ameweka jiwe la msingi katika Shule ya Msingi Flatei Massay iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, kata ya Haydom.
Mkuu wa mkoa ameweka jiwe hilo la msingi katika shule ya Flatei Massay mnamo Agosti 17,2023, katika Halmashauri ya wilaya ya Mbulu kata ya Haydom.
Mheshimiwa Queen amewashukuru na kuwapongeza wananchi wa Haydom kwa ushirikiano na Serikali iliyopo madarakani kwa kuunga mkono juhudi za Serikali zilizowekwa katika kata hiyo ambapo wananchi wamechangia zaidi ya shilingi Milioni kumi na Saba katika ujenzi wa shule ya msingi hiyo. Ambapo Serikali imeweka zaidi ya milioni mia tatu arobaini, ambayo itafanya jumla ya gharama ya ujenzi huo kufika milioni mia tatu sitini na sita.
"Kwa mwaka huu wa fedha, kwenye eneo la Elimu Serikali imetutengea zaidi ya bilioni 5.3 kwa ajili ya muendelezo wa miundombinu kwenye sekta ya Elimu , hii ni ujenzi wa shule Mpya hizi mnazoziona lakini ukarabati wa shule ambazo zimeonekana ni chakavu, nyongeza ya matundu ya vyoo, lakini maboresho ya miundombinu mbalimbali kwenye sekta ya Elimu.Tuendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais Dr. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoipeleka nchi kwenye muelekeo ule ule ambao Watanzania wote wanatamani kukuona." Alisema Mheshimiwa Queen Sendiga.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Komredi Kheri James amesema kuwa baada ya Mheshimiwa Rais Dr. Samia Suluhu Hassan kusikia kilio Cha wananchi wa Mbulu juu ya changamoto ya mrundikano wa wanafunzi katika shule ya msingi ya Haydom, ilimpendeza na aliona ni vyema alete fedha ili tupate shule mpya yenye Kila kitu.
Naye Mkuu wa shule ya msingi Haydom Ndugu Joshua Mwambo John amesema kuwa shule ilipokea fedha kiasi Cha shilingi milioni mia 348 na laki tano kutoka Serikali kuu kupitia mradi wa BOOST.Ambapo fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti ya shule tarehe 24/04/2023 na utekelezaji wa mradi ulianza rasmi Mei 30, 2023.
" Fedha tulizopokea ni kwa ajili ya ujenzi wa shule yenye mkondo mmoja ikiwa na maana ya madarasa mawili ya mfano, vyoo matundu 16, jengo la utawala pamoja na kichomea taka. Lengo la mradi huu Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ni kupunguza mlundikano wa wanafunzi darasani katika shule ya msingi ya Haydom ambayo Ina wanafunzi 1882." Alisema Mwalimu Mwambo
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Ndugu Joseph Mandoo alisema kuwa wananchi wa Mbulu wanayo faraja kubwa sana wanafunzi waliyokuwa wanalundikana zaidi ya elfu moja mia nane, sasa kwa bahati njema chini ya jemedari Flatei Massay kupeleka kilio cha wana Mbulu kwenda kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan kuomba fedha milioni mia tatu arobaini na nane kujenga shule Mpya ya Haydom ambayo ipo mbioni kukamilika, tunaishukuru sana Serikali.
Aidha Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Queen Sendiga baada ya kuweka jiwe la Msingi pamoja na msafara wake wote waliungana na mamia ya wakazi wa Haydom kwenda kuhani na kutoa salaam za rambirambi kwa niaba ya Serikali kufuatia msiba wa mtumishi wa mwenzetu Mwalimu Benedicto S. Nada wa Shule ya Msingi Endaharghadakt kilichotokea mwanzoni wa wiki hii. Kwa pamoja tutaendelea kuyaenzi mazuri yote aliyoyafanya Mwalimu wetu enzi za Uhai, Roho ya Marehemu ipumzike kwa amani. alisema Bi. Queen.
#KWA PAMOJA TUNAIJENGA MBULU YETU#
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.