Eskhesh July 12, 2023.
Afisa ufuatiliaji toka TASAF ndugu. Simon Semetei amewataka walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika kijiji cha Eshkesh, Halmashauri ya Mbulu wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 65 wenye uwezo wa kufanya kazi wajitokeze kufanya kazi katika miradi ya ajira za muda, kwani wanapofanya kazi hizi wajue zinaleta Maendeleo kwenye kijiji na jamii yao ambapo na wao watakua ni sehemu ya wanufaika wa Maendeleo ya Kijiji hicho. Hayo yalisemwa na Semetei wakati akifanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya Ajira za muda inayotekelezwa na walengwa wa TASAF Kijiji Cha Eshkesh.
Miradi ya Ajira za muda kwa Halmashauri ya Mbulu ilianza mwaka 2022 December, ambapo walengwa waliweza kutengeneza Barabara za jamii, Mifereji ya umwagiliaji, visima vifupi, vivuko mbalimbali na malambo ya maji. Miradi hii imewezesha walengwa kupata ujuzi na kuongeza kipato.
Semetei amezungumzia changamoto kubwa waliyokuwa wanailalamikia wanufaika wa mradi, kuhusu ucheleweshaji wa malipo, kuwa dirisha la malipo ya TASAF linaweza kuchelewa kwa sababu mbalimbali ikiwemo uhakiki wa kuthibitisha form zinazoingia mtandaoni kwa ajili ya kuandaa malipo. Pia ulipwaji kwa njia ya kielektroniki unakua na changamoto kwani majina ya mlengwa kwenye Mpango kutofautiana na jina la kwenye namba ya NIDA, hivyo zoezi hilo la uhakiki kupelekea malipo kwa walengwa kuchelewa.
"Niwaombe wanakijiji cha Eshkesh,mjitahidi kuikamilisha miradi iliyo mbele yenu kwa wakati na Kwa kuzingatia ubora na viwango vya kisekta ili miradi iweze kukabidhiwa kwenye Halmashauri na jamii husika "
Aidha kwa upande wake mwezeshaji wa TASAF ngazi ya halmashauri Bi. Debora Amsi alisema kuwa mradi wa pili ambao ni wa upandaji miti, inasubiriwa mvua kuanza kunyesha ili wanufaika waanze kutekeleza mradi kwa kuchimba mashimo na kupanda miti kuzuia upepo. Katika maeneo ya Eshkesh nyumba nyingi zimeezuliwa na upepo kutokana na uhaba wa miti maeneo hayo.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji Cha Eshkesh, Faustini Tlatlaa aliwaasa wanakijiji wakazane kufanya kazi na kushirikiana kwenye mradi. Pia aliwaasa walengwa kutumia pesa wanazopewa kufanyia mambo ya msingi.
“KWA PAMOJA TUNAIJENGA MBULU YETU”
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.