Vijiji sita vya wilaya ya mbulu vyenye wakazi 14,205 vimeanza kunufaika na mradi wa hifadhi jumuishi unaotekelezwa na shirika binafsi la Kimataifa la Uhifadhi wa asili IUCN baada ya kupima na kukabidhi vyeti vya hati miliki ya ardhi ya vijiji.
Vijiji sita vya ukubwa wa eneo la hekta 28,000 vilivyonufaika na mradi huo huo ulioanza mwezi Machi mwaka huu wa 2024 ni Endamilay, Murkuchida, Yaeda Kati, Garbabi, Endalat, Dirim ambavyo sasa vimeepukana na migogoro ya ardhi kati ya vijiji na vijiji na kuwezeshwa kupanga ardhi zao kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Akikabidhi vyeti hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbulu VERONICA KESSY, Katibu Tawala wa wilaya hiyo Paulo Burra ameshukuru shirika hilo la IUCN kufanikisha upimaji huo ambao amesema utapunguza migogoro kati ya vijiji na vijiji kugombea mipaka na pia kati ya wakulima na wafugaji.
Amesisitiza viongozi wa vijiji hivyo kuzingatia matumizi bora ya ardhi kwakuwa maeneo yameainishwa kuzingatia uhitaji wa kila kundi katika vijiji husika hasa maeneo ya malisho na mifugo pamoja na vyanzo vya maji.
Kwa mujibu wa afisa miradi wa shirika hilo la IUCN, Julius Mando, mradi huo unaotekelezwa kwa miaka minne kuanzia mwezi Machi mwaka huu wa 2024 hadi 2027 unagharimu shilingi milioni 700 za kitanzania ukijumuisha upimaji wa ardhi na utoaji wa elimu kwa viongozi wa serikali za vijiji na kuwezesha wanawake kujua haki na wajibu wao kupitia mabaraza yao.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ndugu Nicolaus Ngonyani ameomba taasisi hiyo kufikiria uwezekano wa kuendelea kujumuisha vijiji vingine vya Halmashauri hiyo ili viweze kunufaika na mradi huo.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.