MBULU-MANYARA
Jamii mkoani Manyara imetakiwa kuzingatia makundi muhimu ya vyakula kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito ili kukabiliana na hali ya udumavu na uzito mdogo kwa watoto inayokabili mkoa huo ambao takwimu zinaonesha asilimia 32 ya watoto imedumaa.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa mkoa wa Manyara QUEEN SENDIGA katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa wilaya ya Mbulu VERONICA KESSY katika maadhimisho ya siku ya Lishe mkoa wa Manyara iliyofanyika wilayani MBULU.
Kwa mujibu wa Utafiti wa hali ya lishe nchini uliofanywa na Tanzania Demographic Survey mwaka 2022, asilimia 32 ya watoto wenye umri wa mwaka 0 hadi miezi 59 mkoani Manyara wamedumaa, asilimia 19.6 wana uzito mdogo na asilimia 4.7 wana ukondefu.
Hiyo ndiyo iliyosukuma wizara ya afya kufanyia maadhimisho hayo mkoani MANYARA kushirikiana na shirika la TAHA wakitumia wataalamu wa lishe kutoa elimu ya lishe pamoja na kuhimiza kilimo cha mbogamboga na wanyama wadogo kwa ajili ya matumizi kaya ili kukabiliana na udumavu.
Mkuu wa wilaya ya Mbulu VERONICA KESSY licha ya kuhimiza Wananchi kilimo cha mbogamboga pamoja na ufugaji wa wanyama wadogo kwa ajili ya matumizi ya chakula cha kaya pia amekemea tabia ya unywaji pombe haramu ya gongo hasa kina mama kuwanyesha watoto pombe kwa lengo la kuwafanya wapate usingizi ili wafanye shughuli zao kwamba kufanya hivyo ni hatari kwa afya ya watoto kwani wanatengeneza usugu wa pombe na kuwadumaza watoto.
Kaimu afisa mtendaji mkuu wa TAHA ANTONY MANGA ametoa wito kwa jamii mkoani humo kujenga mazoea ya kula makundi yote muhimu ya vyakula ili kukabiliana na hali ya udumavu, uzito mdogo na ukondefu.
Pia ameahidi kuwa TAHA itashirikiana na wilaya hiyo kuanzisha kilimo cha zao la Parachichi kutokana na hali ya hewa ya wilaya hiyo kuruhusu zao hilo kustawi na kwamba hiyo itachangia kuongeza kipato cha wanafamilia na mkoa huo.
"Tunashukuru wafadhili wetu shirika la kimataifa la maendeleo la serikali ya SWEDEN kutuwezesha kuandaa siku hii na kugusa maisha ya jamii kupitia elimu ya lishe"
Kijiji cha LAGANGESH kilichopo katika kata ya YAEDA HHAMPA yalikofanyika maadhimisho hayo ni moja ya eneo ambalo hali ya lishe ni duni zaidi.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu, PETRO TARMO ameshukuru kwa fursa hiyo ya kupewa elimu katika maadhimisho hayo yaliyoambatana na maonesho ya makundi mbalimbali ya vyakula pamoja na upimaji bure wa afya na ushauri kuhusu lishe kutoka kwa wataalamu mbalimbali wa TAHA, wizara, mkoa na wilaya.
Naye Diwani wa viti maalum, NURUANA KIPAPAI amesema atatumia elimu aliyopata katika maadhimisho hayo kwenda kuelimisha jamii kupitia mikutano mbalimbali.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya siku ya lishe mwaka huu ni "Lishe bora kwa afya njema na ustawi wa Taifa"
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.