Na, Ruth Kyelula, Mbulu DC,
Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mbulu, Reginah Msigwa ameitaka jamii kutambua, kuthamini uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta maendeleo, kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo yao, familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla.
Mgeni rasmi Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mbulu, Reginah Msigwa, akisoma hotuba yake kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake, Maghang Mbulu.
Hayo yalisemwa na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mbulu, Reginah Msigwa wakati akisoma hotuba yake ambayo alimwakilisha mgeni rasmi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Kheri James, katika viwanja vya Maghang, wilayani Mbulu, March 08, 2024.
“Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imetekeleza yafuatayo katika kuhakikisha kuwa wanawake wanastahili kwa kufanya mambo mbalimbali yakiwemo: kuwashirikisha wanawake katika chaguzi zote za vyama vya siasa, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, kutenga na kutoa asilimia 4 ya mapato ya ndani ya Halmashauri na kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali bila riba na kuhakikisha kuwa mimba mashuleni zinakomesshwa katika shule za msingi na sekondari.” Alisema Hakimu Reginah.
Wanawake wa Wilaya ya Mbulu kwenye picha ya pamoja katika viwanja vya Maghang, Mbulu
Naye mwakilishi wa Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Mbulu, Mheshimiwa Agness Karengi, alisema kuwa wanawake wa Wilaya ya Mbulu wajitahidi kuupinga ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kijinsia ambao upo na unafanyika katika jamii zetu, alisema itoshe sasa kunyanyasana na wanyanyasaji waibuliwe wasifumbiwe macho.
Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Praxeda Kanja, alisema kuwa anawashukuru wanawake wa Wilaya ya Mbulu kwa kuitendea haki siku ya wanawake, walijitokeza kwa wingi na anaamini ujumbe kwa wanawake ulifika na pia imeonesha mwamko fulani kwa jamii.
“Katika maadhimisho hayo kulikuwa na matukio mbalimbali ya kijamii, kama upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi na ugawaji wa Taulo za kike katika shule ya sekondari Maghang, kwahiyo siku yetu kwa ujumla iligusa maeneo mengi.” Alisema Kanja.
Aidha Praxeda alitoa wito kwa wanawake wa Wilaya ya Mbulu na Tanzania kwa ujumla kuwa wanawake waendelee na shughuli mbalimbali ambazo zinawasababisha wasonge mbele, lakini pia wakatae mila na desturi ambazo ambazo zinagandamiza maendeleo ya mwanamke au kuondoa utu wake kama mwanamke, hususani vitendo vya ukeketaji.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.