Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dokta Suleyman Jafo amewataka wamiliki wa biashara ya Carbon Tanzania wafanye mgawanyo wa hela sambamba na kanuni ya nne ya Carbon kipengele cha C, ya uwazi katika biashara ya Carbon na ijulikane tani ngapi zimeenda kuuzwa na kwa kiasi gani.
Hayo yalisemwa na Waziri Jafo katika kikao cha kukabidhi cheki ya bilioni 4, 740, 7000.00 ikiwa ni faida ya biashara ya hewa ukaa inayofanyika kwa uhifadhi wa misitu na mazingira chini ya usimamizi wa Taasisi ya Carbon Tanzania kwa wilaya nufaika za miradi huo ambazo ni Wilaya ya Mbulu na Wilaya ya Kiteto, kilichofanyika katika ukumbi wa White Rose Babati, Mkoani Manyara Novemba 14, 2023.
“Tulitoa maelekezo ya kampuni zote zinazoshiriki biashara ya Carbon, kwanza zifanye usajili/registration, na mpaka leo hii ninavyozungumza Zaidi ya makampuni 33 yameshajisajili katika biashara ya Carbon nchini Tanzania, na katika makampuni hayo, makampuni 12 tumeshayapa no objection letter. Na kampuni ya Carbon Tanzania tumeshawapa endorsement letter, hongereni sana.” Alisema Waziri Jafo.
Aidha Waziri Jafo alisema kuwa serikali inataka watu wabadilike,na kuongeza katika biashara hii ya Carbon wanatarajia kwanza ajira nyingi zipatikane katika maeneo ya wakazi wa mradi na itakuwa ni fursa ya ajira.Lakini pili pato litakuja kwenye Serikali itakayokuwa inahudumia wananchi kwa rasilimali zake zilizokuwa nazo.
Waziri Jafo amewapongeza na kuwasifu Carbon Tanzania kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya,lakini pia amewaomba maarifa mengine ya uwazi na utunzaji wa kanuni waifanyie kazi katika toleo lijalo la mgao.Pia amewaomba wananchi watunze misitu yao kwa sababu misitu ni mali na agenda ya kutunza mazingira ni agenda ya kudumu kwetu sote.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema kuwa anawashukuru sana watu wa Carbon Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuona umuhimu wa kufanya shughuli hii leo na ni kwa mara ya kwanza tumekusanya kusanyiko kama hili la wanufaika na kuweza kuwapatia fedha hizi wao wenyewe moja kwa moja mbele yako wewe Waziri mwenye dhamana.
Kwa upande mwengine RC queen amesema kuwa wamepata faida nyingi kupitia mradi huo ikiwemo utunzaji wa mazingira,utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi.Faida ambayo tunapata ni kubwa sana na kwa wenzetu kule Mbulu wameendelea kupata hii faida katika vijiji vitano,na mradi umeendelea kutoa matokeo mazuri.Eneo ambalo limetengwa kule ni Zaidi ya hekta laki moja na kumi ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi.Na wanufaika wa mradi huu ni Zaidi ya watu elfu sitini na nne katika mradi huu ambao wameendelea kupata faida ya kuboreshewa huduma za kijamii.
Naye Mkuuu wa Wilaya ya Mbulu Kheri James amesema kuwa kwa mara ya kwanza tunaanza kuwaona watoto wanaotoka katika jamii za wafugaji wanasoma kwenye shule nzuri,wanapata elimu bora na kwa viwango wanavyovitaka,na wengine wapo hadi vyuo vikuu kupitia program hii.Lakini pia inawasaidia kuwa sawa kwenye soko la ushindani wa ajira, lakini unyonge huo umeondoka.
Aliendelea kusema kuwa pamoja na faida hizo za kimazingira, mpango huu wa uvunaji wa hewa ya ukaa umechochea matumizi bora ya ardhi ndani ya Wilaya.Na mpango wa ardhi unapoimarika unatusaidia kupunguza migogoro ya ardhi.Aidha biashara ya hewa ukaa katika Wilaya ya Mbulu ipo katika maeneo ya Yaeda chini, Mongo wa mono, Domanga, Eshkesh na Endanyawish.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Fedha wa Carbon Tanzania, Alphael Jackson amesema kuwa mradi wa hewa ya ukaa katika bonde la Yaeda ulianza mwaka 2013 ikiwa chini ya Halmashauri ya Mbulu,ikihusisha jamii za Wahadzabe, mongo wa mono,Domanga na Yaeda chini.Na tulianza na vijiji viwili lakini tulilenga Zaidi upande wa Wahadzabe.
Aliendelea kusema kuwa mradi unahusisha misitu iliyopo ndani ya vijiji kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi,yenye ukubwa wa hekta laki moja na kumi mia tano ishirini na sita na yenye jumla ya wakazi elfu sitini na nne wanaonufaika na mradi huu wa hewa ukaa.
“Mradi una lengo la kuhifadhi mazingira,sisi tunaangalia misitu Zaidi na ni misitu ya asili,kutunza vyanzo vya maji,mradi umelenga kuboresha huduma kwa jamii katika kuhifadhi na kunufaika moja kwa moja na faida za uhifadhi.”Alisema Alphael.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.