Mbunge wa Mbulu vijijini Mheshimiwa Flatei Massay amemshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia fedha nyingi Mbulu vijjijini ambazo zimeweza kutatua kero nyingi za wananchi.
Mbunge wa Mbulu vijijini Mhe. Flatei Massay akiongea na Baraza la Madiwani la bajeti ya fedha 2024/2025.
Hayo yalisemwa na Mbunge wa Mbulu vijijini mhe. Flatei Massay wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani cha Bajeti ya fedha 2024/2025, jana Februari 08, 2024, katika ukumbi wa Halmashauri, Dongobesh, Mbulu.
“kwa miaka mitatu na nusu hii tumepata jumla ya madaraja kumi na nane, Kwa upande wa maji tumepata jumla ya shilingi bilioni 41 ambayo tangu Mbulu imeanzishwa hatujawahi kupata fedha kama hizo. Na kwa upande wa sekta ya mifugo kwa mwaka jana na mwaka huu, tumepata majosho kumi na tano. Ni jambo la kumshukuru sana Mhe. Rais.” Alisema Mh. Flatei.
Kwa upande wa Katibu Tawala wa Wilaya, Paulo Bura amewataka TARURA na TANROADS ndani ya siku saba wawe wamelifanyia kazi dimbwi ambalo limesababisha vifo vya watu watatu (wanafunzi wawili na mtu mzima mmoja) katika kata ya Dongobesh kijiji cha Qaloda.
“Nimepeleka mwenyewe barua TANROADS na TARURA, ili waone nini ambacho kinaweza kufanyika kwa sababu hilo dimbwi lipo karibu sana na shule ya msingi Qaloda lakini pia lipo katikati ya makazi ya watu. Tumeshapoteza watatu hatutaki kupoteza tena wananchi zaidi.” Alisema Katibu Tawala Bura.
Aliendelea kusema kuwa anamuunga mkono Mh. Mbunge kwa kumshukuru Mhe. Rais kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo na uendeshaji, na kuwasihi wataalamu kusimamia miradi ikamilike kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, Joseph Mandoo, alisema kuwa Baraza la Madiwani la bajeti ya fedha 2024/2025, limepitisha mpango wa mapendekezo ya bajeti ambao ni bilioni 34,932,922,400.00.
Mhe. Mandoo alimpongeza mbunge wa Mbulu vijijini mhe. Flatei kwa namna alivyowawakilisha vizuri kwenye bunge la Jamuhuri ya Tanzania na kujibu kiu ya wana Mbulu, kuhakikisha mpango wa maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu unafikiwa na bunge, na fedha zinaletwa. Huo wote pia ni mchango wake mkubwa, ambao unatufanya sisi Madiwani kwenye kata zetu tuwe na miradi mingi chini ya Mhe. Rais, Mbunge na mapato yetu ya ndani ya Hamashauri.
Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri, Abubakar Kuuli, alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, wamejipanga vizuri kwenda kuongeza uwezo wa Halmashauri kujitegemea.
“Tunaenda kuweka miradi ya kimkakati, tutasimama kidogo kupeleka huko kwa wananchi, ili tuweke miradi ambayo hata siku serikali ikisema Halmashauri ijitegemee, angalau tutakwenda hata miezi nane.Tunaweza tukalipa mishahara,umeme,maji,tukaendesha magari yetu, tukakarabati, kila kitu angalau kwa miezi nane.Kwahiyo kuna mikakati mikubwa tumeiweka kwa ajili ya kuweka vitu ambavyo vitakuwa vinatuingizia mapato mengi Zaidi.” Alisema Kuuli.
Kamati ya Usalama ya Wilaya, wakisikiliza hoja mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kwenye Baraza hilo.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.