Na, Ruth Kyelula Mbulu DC,
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Veronica Kessy, amewataka wananchi wa kata ya Endamilay, wale wote ambao wamejiandikisha katika kata hiyo ambao ni 7,720 wakapige kura ifikapo Novemba 27,2024.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Veronica Kessy akiwa na timu ya wataalamu toka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wataalamu kutoka Halmashauri.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Veronica Kessy wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Endamilay katika ziara yake, Novemba 21,2024.
Aidha Mhe. Kessy aliwaambia wananchi hao ujio wa mradi mkubwa wa umwagiliaji unaotarajiwa kuanzishwa katika kata ya Endamilay, na kuwaambia waanze kujiandikisha katika ofisi za kata kama maelekezo yanavyowataka.
“Huu mradi utakuwa mradi mkubwa wa umwagiliaji kwa sisi wana Endamilay, huu mradi utakuwa ni mradi wa umwagiliaji ambapo wataalamu wataandaa mpango wa matumizi ya ardhi hiyo kwa ajili ya umwagiliaji, kwa sababu ni mradi wa maendeleo yetu sisi, ipo ardhi itahitajika kwa ajili ya kuchimba na kujenga bwawa ili tuweze kuyakinga na kuyakusanya maji na wataalamu hao wataanisha maeneo ya kujenga bwawa na maeneo ambapo mifereji itapita na ujumla wa eneo ambapo kitalimwa hicho kilimo cha umwagiliaji.” Alisema Mhe. Kessy.
Diwani wa Eshkesh Bajuta akizungumza na wananchi wa Endamilay mara baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mbulu kuwasili
Aliendelea kusema kuwa kikubwa wananchi wanachopaswa kujua ni mradi huo ni kwa ajili ya maendeleo yao na kilimo kinaenda kuboreshwa, kwamba wanapokuwa na maji wanakuwa na uhakika wa kulima hata mara tatu kwa mwaka. Lakini pia wataalamu wa kilimo watawaambia ni mazao yapi yatafaa kwa wakati gani katika hiyo scheme ya umwagiliaji.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Veronica Kessy, akizungumza na wananchi wa Endamilay mara baada ya kuwasili
Kwa upande wa Fundi sanifu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa Wilaya ya Mbulu, Jackline Kalebu,alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuendeleza na kuongeza uzalishaji wa kilimo cha uhakika, kuinua uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Fundi sanifu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa Wilaya ya Mbulu, Jackline Kalebu akizungumza na wananchi wa Endamilay kuhusu mradi mpya wa umwagiliaji.
Alisema kuwa mradi huo wapo kwenye hatua za mwanzo, ya uibuaji wa miradi, kujua eneo lipi litafaa kwa ajili ya umwagiliaji. Lakini pia alisema sheria za Tume zinataka scheme zote za umwagiliaji zisajiliwe, ili zitambulike kisheria na wapate mradi huo.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.