Na, Magreth Mbawala, Mbulu DC.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Abubakar Kuuli amewaasa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kutokomeza ukatili wa kijinsia kwenye jamii.
Haya yamesemwa leo tarehe 08/10/2025 katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu akiwa anafungua mafunzo ya siku 3 kuhusiana na ukatili wa kijinsia yaliyoandaliwa na Kanisa la KKKT kupitia kitengo cha ustawi wa jamii.Mafunzo hayo yametolewa kwa kata mbili za Eshkesh na Yaeda Chini.
Mkurugenzi Kuuli aliwataka wote waliohudhuria semina kwenda kuwaelimisha na kuwafundisha wengine kwenye jamii zao madhara makubwa ya ukeketaji kwani jambo hilo ni kumkosesha mtoto wa kike haki yake ya msingi lakini pia linasababisha kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua na kusababisha kifo.
“Ndugu zangu hali yetu ni mbaya kama Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwenye swala zima la ukeketaji,mmekusanywa hapa kwa ajili ya kupokea semina na maelekezo kwakua kitendo kinachofanyika katika jamii yetu sio kitendo kizuri hata kidogo.”Alisema Kuuli.
Naye mwezeshaji wa kitaifa maswala ya ukatili wa kijinsia Faith Dewasi, amesema mabinti wengi waliofanyiwa ukatili wa ukeketaji wameathirika kisaikolojia na kushindwa kuendelea na masomo,wameshindwa kuingia na jamii hivyo ndoto zao zinakua zimefutwa.
Pia Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Emma Ngatoluwa, alisema mkoa wa Manyara unashika nafasi za juu kwenye swala la ukatili wa kijinsia,na ukeketaji kwa Mkoa wa Manyara upo kwa asilimia 43 kutokana na sensa ya mwaka 2022/2023.Tathmini inaonyesha kata za Eshkesh na Yaeda Chini zinaongoza kwa matendo ya ukatili wa kijinsia.
Mwisho mratibu wa Kurugenzi ya afya ya diakonia makao makuu ya KKKT Ezekiel Massawe alisema waliomba fedha kutoka kwa wafadhili ili kuweza kufanya utafiti kwa miezi 3 katika kata hizo mbili ambazo ukatili umekithiri. Wamewaita viongozi wa kiserikali,kimila,wakunga wa jadi,viongozi wa kidini na wazee maarufu ili kushirikiana nao kwa pamoja katika kutoa Elimu hiyo kwenye jamii zao.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.