Kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imehitimisha kikao chake cha robo ya pili (Oktoba–Desemba, 2025) kwa mafanikio makubwa, huku ikipitisha maazimio mapya yaliyojikita katika kuboresha hali ya lishe kwa watoto, wanawake wajawazito, na jamii kwa ujumla.
Kikao hicho, kimefanyika mapema hii leo 09/01/2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri kilichowashirikisha wajumbe wa kamati kutoka sekta ya afya, elimu, kilimo, na wadau mbalimbali wa lishe. Wajumbe walikagua maendeleo yaliyopatikana katika kipindi kilichopita na kuangalia changamoto zilizopo ili kuhakikisha mpango wa lishe unatekelezwa kwa ufanisi.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao, Mwenyekiti wa kikao ndugu Elifadhili Manairi, amesema kuwa kikao kimekuwa na tija kubwa kwani kila idara imetoa taarifa za maendeleo na mapendekezo ya utekelezaji wa sera za lishe. Amebainisha kuwa maazimio yaliyopitishwa yanahusisha kuimarisha upatikanaji wa chakula bora shuleni, kuongeza kampeni za lishe kwa wanawake wajawazito, na kuhakikisha mifumo ya ufuatiliaji wa lishe katika jamii inakamilika.
“Tunajivunia mafanikio tuliyoyapata katika robo hii ya pili. Huu ni mwanzo mzuri wa kuendeleza mpango wetu wa kuhakikisha lishe bora inapatikana kwa kila mtoto na kila mwanamke mjamzito katika Halmashauri yetu,” alisema Manairi
Aidha, Kamati imesisitiza umuhimu wa kushirikiana na wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha maazimio yanatekelezwa ipasavyo sambamba na Kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye lishe mashuleni na katika jamii, Kuimarisha elimu ya lishe kwa wazazi na walimu, Kuweka mifumo ya ufuatiliaji wa hali ya lishe kwa watoto na wanawake wajawazito, Kushirikisha wadau mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji
Kikao cha robo ya pili cha mwaka 2025/2026 kimeonyesha dhamira ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kuhakikisha lishe bora inapatikana kwa wote, na kuimarisha juhudi za maendeleo endelevu. Hii ni ishara tosha kwamba Halmashauri inachukua lishe kuwa kipaumbele kikuu katika ajenda yake ya maendeleo ya jamii.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.