Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imepongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hii, ikieleza kuridhishwa na matumizi sahihi ya fedha pamoja na ubora wa kazi unaoonekana katika maeneo mbalimbali.
Pongezi hizo zimetolewa leo 07/01/2026 Wakati wa ziara ya robo ya pili ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani, fedha kutoka Serikali Kuu na Wahisani ikiwa ni sehemu ya jukumu la kamati kuhakikisha thamani ya fedha inalindwa na miradi inakamilika kwa viwango vilivyokusudiwa.
Akizungumza kwa niaba ya kamati, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango Mhe. Yeconia Deless amesema kuwa miradi mingi iliyotembelewa ipo katika hatua nzuri za utekelezaji na inaonesha kuzingatia mipango, bajeti na muda uliopangwa.
“Kamati imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi tuliyotembelea. Tunazipongeza idara husika, wasimamizi wa miradi pamoja na wakandarasi kwa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia mkataba,” alisema Mhe. Deless.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ndugu Juma Kilimba ameeleza kuwa halmashauri itaendelea kusimamia miradi yote kwa karibu ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika, huku akitoa wito kwa watendaji na wakandarasi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uwajibikaji.
“Nichukue fursa hii kuishukuru Kamati ya Fedha kwa maelekezo na ushauri walioutoa. Halmashauri itaendelea kuyafanyia kazi ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha wananchi wananufaika kikamilifu na miradi ya maendeleo,” alisema Kilimba
Ziara hii ni sehemu ya ratiba ya kawaida ya kamati katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.