Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Mhe. Michael Semindu, ameongoza zoezi la upandaji miti 400 katika Shule ya Amali Harsha na kituo cha Afya Dongobesh, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhe. Semindu amesisitiza umuhimu wa jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwa kupanda na kutunza miti, akibainisha kuwa miti ni nguzo muhimu katika kulinda vyanzo vya maji, kuboresha hali ya hewa na kuhakikisha maisha endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho ambapo Wilaya ya Mbulu inatarajia kupanda Miti 1,500,000 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.
“Uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu. Kupanda miti leo ni kuwekeza kwenye maisha ya baadaye ya watoto wetu,” alisema Mhe. Semindu.
Aidha, amewahimiza walimu wa shule hiyo kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa ipasavyo ili iweze kukua na kuleta tija iliyokusudiwa. Aliongeza kuwa shule ni maeneo muhimu ya kuanzia kujenga kizazi chenye uelewa na uwajibikaji wa masuala ya mazingira.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Mhe. Dkt Emmanuel Nuwas naye ameshiriki kikamilifu na kupongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu katika kulinda mazingira, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, viongozi na wananchi ni msingi wa mafanikio ya uhifadhi wa mazingira.
“Ni wajibu wetu sote, viongozi na wananchi, kuhakikisha tunalinda mazingira kwa vitendo. Upandaji miti katika shule ni hatua muhimu ya kujenga kizazi chenye uelewa na uwajibikaji wa mazingira,” alisema Nuwas
Pia Uongozi wa shule umeishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa mazingira na kuahidi kushirikiana na wanafunzi katika kutunza miti hiyo kama sehemu ya mafunzo ya vitendo.
Zoezi hilo la upandaji miti ni sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya Serikali ya kulinda mazingira chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imeendelea kuhamasisha upandaji miti katika shule, vituo vya afya na maeneo ya umma ili kuhakikisha Wilaya inaendelea kuwa ya kijani na salama kwa maendeleo endelevu
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.