
Na. Nashon Biseko, MDC
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Michael Semindu amewataka Madiwani kuitunza thamani waliopewa na Wananchi kwani thamani hii ni deni la kuaminiwa katika utatuzi makini wa changamoto zao na kuwapelekea Maendeleo.
Amesema hayo katika kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani kilichofanyika 02/12/2025 Katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kilichohusisha Uapisho wa Waheshimiwa Madiwani, Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, kuunda kamati za kudumu za Halmashauri, Kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa kipindi cha Julai hadi Novemba na kupitisha ratiba ya vikao vya Halmashauri.
Aidha Diwani wa Kata ya Haydom Mhe. Yeconia Maleyecky kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amechaguliwana Baraza la Madiwani kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu baada ya kupata kura zote za ndio 24 zilizopigwa na Wajumbe wa baraza hilo, Pia Diwani wa Kata ya Masqaroda Mhe.Petro Slaa Tarimo ameibuka mshindi kwa kura zote za ndio 24 kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu.
Pia Mhe. Semindu amelitaka Baraza la Madiwani kuhakikisha wanawazingatia vijana katika ajira rasmi na zisizo rasmi, kuwawezesha kibiashara, kuwasikiliza na kuwashirikisha katika maamuzi ili kujenga taifa imara.
“Ndugu zangu niwakumbushe katika taifa letu jamii kubwa ya Wapiga kura wetu kati ya asilimia 67 hadi 70% ni vijana waliozaliwa enzi za Mzee Mwinyi akiwa anatoka madarakani kwahiyo tunapopanga mipango yetu kama Halmashauri ni lazima tuwazingatie katika mahitaji, Matakwa, nafasi, maombi muhimu, ajira rasmi na zisizo rasmi, kutambuliwa, kushauriwa katika biashara na miradi, kusikilizwa na kupewa kipaumbele katika kazi za manunuzi ili tuwe na uhakika wa chaguzi zetu zijazo”. Alisema Semindu
Pia Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Mhe. Dkt Emanuel Nuwas amewapongeza Madiwani wote kwa kula kiapo tayari kwa kuanza majukumu yao ya kuwatetea wananchi sambamba na kumpa ushirikiano mhe. Rais, Mawaziri, Wabunge na viongozi wote ili kufikia malengo yetu.
“Naomba tumpe ushirikiano Mhe. Rais, Baraza la Mawaziri, Mbunge, Madiwani na Viongozi wengine ili waweze kutekeleza majukumu yao katika kuwatetea Wananchi, kuwaletea maendeleo, kusimamia amani na kuhakikisha tunajenga amani ya Tanzania, utu wa Mtanzania hasa katika jimbo la Mbulu Vijijini”. Alisema Nuwas
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mhe. Yeconia Maleyecky amesisitiza suala la ushirikiano kwani kwa kushirikiana kwa Pamoja itatusaidia kufanya kazi zetu vizuri na kwa ufanisi mkubwa.
“Jahazi hili ni kubwa tunahitaji ushirikiano ili kufanikiwa kwani hakuna mtu anayejua kilakitu lakini tukiungana kwa Pamoja kila mtu akatoa mchango wake hakika tutafikia malengo yetu na kwa ufanisi kama Halmashauri”. Alisema Maleyecky
Pia Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye ni Katibu wa Baraza la Madiwani Ndg. Abubakary Kuuli amelishukuru Baraza na uongozi uliopita kwa ushirikiano mkubwa na amelitaka baraza jipya na uongozi wake kutoa ushirikiano wa dhati ili kufikia malengo na mafanikio ya Jimbo la Mbulu Vijijini.



Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.