Na, Ruth Kyelula & Magreth Mbawala, Mbulu DC.
Rais Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za mwaka mpya 2025 kwa watoto wenye mahitaji maalumu, shule ya msingi Dongobesh Viziwi, ili washiriki sikukuu ya mwaka mpya kwa furaha.
Zawadi hizo zimetolewa leo Desemba 31,2024 na Katibu Tawala wa Wilaya, Paulo Bura, ambae amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Kwa niaba ya Mhe. Rais Dk. Samia kwenye Shule ya Msingi Dongobesh Viziwi, iliyopo kata ya Dongobesh, Mbulu.
“Jambo la kwanza nimeelekezwa nifikishe salamu za Mhe. Rais kwenu wana Dongobesh, kwamba yupo pamoja nasi wana Dongobesh na wana Mbulu kwa ujumla, katika kusukuma gurudumu la maendeleo lakini pia nimeshukuru kuwaona wawakilishi wa wanafunzi wapo na ndio tutawapa hizi bidhaa ambazo ameziandaa yeye mwenyewe.” Alisema Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbulu, Bura.
Alisema Mhe.Rais anawashukuru hususani waalimu wa shule hii ya viziwi ya Dongobesh kwa jinsi wanavyoendelea kuwaandaa wanafunzi hawa wenye mahitaji maalumu na ambao wanahitaji taaluma ya kipekee.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, Joseph Mandoo, alisema kuwa anamshukuru Mhe.Rais kwa namna anavyoendelea kuwahudumia watanzania wa maeneo mbalimbali, hasa kwenye hii Nyanja ya kuwasaidia watoto wenye uhitaji, na hasa shule ya Dongobesh Viziwi ina uhaba wa chakula kama wanavyofahamu, na wakaona ni vema kupitia agizo la Mhe. Rais kuwapeleka chakula.
Katibu Tawala, Paulo Bura, amekabidhi Mbuzi mmoja, chumvi, mchele, sukari, sabuni ya mche na ya unga, mafuta ya kupikia na Maharage.
“Kipekee nipende kumshukuru Mhe.Rais na kumpongeza kwa namna ameweza kuwajali watoto wetu wa Tanzania wakiwepo hawa wa shule ya msingi Viziwi Dongobesh.” Alisema Mandoo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakar Kuuli, alisema kuwa kuna haja ya kila mmoja kuangalia kwenye maeneo wanaoishi, wahitaji ambao wanaweza kuwapa zawadi ya chakula kwa siku ya mwaka mpya hata kama ni kilo moja ya mchele na kilo moja ya nyama ili nao wafurahie mwaka mpya, na itakuwa ni moja ya kumuunga mkono Mhe.Raisi.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.