Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imeendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo ya Asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Katika awamu hii, jumla ya Shilingi 274,956,399.76 zimetolewa kwa vikundi 44, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Halmashauri wa kukuza shughuli za kiuchumi, kuongeza kipato cha kaya na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Mbulu.
Akizungumza wakati wa zoezi la utoaji wa mikopo hiyo, uongozi wa Halmashauri umeeleza kuwa mikopo ya Asilimia 10 inalenga kuwajengea uwezo wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali, ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara ndogondogo na shughuli nyingine za kiuchumi.
Aidha, wanufaika wa mikopo hiyo wameaswa kutumia fedha walizopokea kwa malengo yaliyokusudiwa, kusimamia miradi yao kwa uadilifu na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kunufaika na mpango huo muhimu.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu itaendelea kutoa elimu kwa vikundi kuhusu usimamizi wa fedha, uendeshaji wa miradi na umuhimu wa nidhamu ya urejeshaji wa mikopo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo chanya na endelevu kwa maendeleo ya wananchi.
Mpango wa mikopo ya Asilimia 10 ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya Awamu ya Sita inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi, kupunguza umaskini na kujenga jamii yenye ustawi na maendeleo endelevu.
Mbulu district Coucil
Anuani: P.O.BOX 74
Simu ya mezani: +255743583078
Simu: +255716992222
Barua pepe: md@mbuludc.go.tz
Copyright ©2018 Mbulu District Council . All rights reserved.